Loading...


 

SEHEMU YA 1: UTANGULIZI

Dubbing Development Group (DDG) ni kikundi cha wasanii wanaonakirisha sauti waliokusudia kuunganisha nguvu zao pamoja ili kupambana na umaskini na hatimaye kuongeza kipatao kupitia shughuli mbali mbali za kisanaa na ujasiliamali. Kikundi kimeanzishwa kikiwa na wanachama waliolenga kujiletea maendeleo, hivyo kuweza kukidhi mahitaji ya msingi ya wanachama katika shughuli za maendeleo

IBARA YA 1: JINA LA KATIBA

Katiba hii inajulikana kama ‘katiba ya kikundi cha  DUBBING DEVELOPMENT GROUP kilianzishwa mwaka 2019.

SEHEMU 2: JINA, ANUANI YA KIKUNDI

IBARA YA 2: JINA LA KIKUNDI

Kikundi kinajulikana kwa jina la DUBBING DEVELOPMENT GROUP.  Kwa kifupi D.D.G

IBARA 3: OFISI NA ANUANI YA KIKUNDI

Ofisi na Makao makuu ya kikundi yapo Nyumba namba……………… mtaa…………………. kata ya …………… Wilaya ya …………………., 

Anuani ya posta S.L.P ………. Kinondoni, Mkoa wa Dar es salaam.

IBARA YA 4: ENEO LA SHUGHULI ZA KIKUNDI

Shughuli za kikundi zitafanyika Tanzania nzima bara na visiwani

IBARA YA 5: LUGHA

Lugha inayotumika ni kiingereza na Kiswahili.

 

SEHEMU YA 3: MADHUMUNI YA SHUGHULI ZA KIKUNDI

IBARA 6: MADHUMUNI YA KIKUNDI

a)   Kuwezesha wanachama kujikwamua kiuchumi

b)   Kuanzisha msingi wa kuwa na vyanzo vingi vya mapato ili kujiongezea kipato.

c)   Kukopeshana fedha yenye masharti nafuu

d)   Kushirikiana na kusaidiana katika raha na shida.

IBARA YA 7: SHUGHULI ZA KIKUNDI

a)   Kushirikiana na kusaidiana

b)   Kuelimisha wanachama elimu ya biashara na ujasiliamali

c)   Kulinda na kutetea maslani ya wasanii wanakilisha sauti Tanzania(Dubbing artist)

SEHEMU YA 4: UANACHAMA

IBARA 8: TARATIBU ZA UANACHAMA.

Kikundi kitakuwa na wanachama waanzilishi ambao watakuwa ndio waliounda wazo hili kwa pamoja ambao wamekidhi vigezo na sifa ya kuwa wanachama. Idadi ya wanachama inaweza kuongezeka kadri wanachama wapya watakavyojitokeza.


IBARA 9: AINA YA WANACHAMA

a)   Kutakuwa na wanachama waanzilishi ambao wameshiriki kuandaa katiba hii na wamelipa kiingilio cha Tshs 50,000/=

b)   Kutakuwepo na wanachama walezi iwapo wanachama wataona umuhimu wa kufanya hivyo.

c)   Wanachama watakaoingia baada kikundi kuundwa watapaswa kulipa kiingilio cha shilingi 50,000/= Pamoja na jumla ya michango yote iliochangwa na wajumbe wengine

 

IBARA 10: SIFA YA UANACHAMA

Mtu yeyote anaweza kuwa mwanakikundi anapokuwa na sifa zifuatazo: -

a)    Awe mtu anayehusiana na sanaa za unakirishaji sauti

b)   Awe mwenye kutunza siri za kikundi.

c)    Awe na umri wa miaka 18 na kuendelea.

d)   Awe anakubaliana na masharti ya katiba hii na kuifuata.

e)    Awe ameshiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi zinazoendeshwa na kikundi.

f)     Awe na akili timamu.

g)   Awe mwenye tabia njema, anayejituma na anayejiheshimu.

h)   Awe mwenye uelevu yakinifu unaokusudia maendeleo.

i)     Awe mchapa kazi na mbunifu.

j)     Awe mwaminifu.

 

 

IBARA 11: HAKI ZA MWANACHAMA

a)    Kugombea uongozi na kuchaguliwa au kuchagua viongozi anaowaona wanafaa.

b)   Kujieleza na kujitetea anaposhutumiwa hatua kwa hatua mbele ya kamati ya utendaji, mikutano ya kikundi au uongozi wa serikali.

c)    Kupata taarifa zote za masuala ya kikundi na kuhoji maendeleo ya kikundi.

d)   Kupewa hadhi na huduma sawa na wenzake bila upendeleo.

e)    Kupata mkopo pindi atakapohitaji.

f)     Kila mwanakikundi anayo haki ya kupewa gawio sawa na mapato ya kikundi na taratibu za kikundi.

g)   Kukemea ukiukwaji wa kanuni na taratibu za katiba kwa viongozi

 

IBARA 12: WAJIBU WA MWANACHAMA

Wanakikundi wote watakuwa na wajibu na majukumu yafuatayo: -

a)    Kuhudhuria na kushiriki katika vikao vyote halali kwa mujibu wa katiba.

b)   Kutoa michango yote halali kama ilivyoanishwa na katiba pamoja na michango mingine itakavyokubaliwa na wanachama kwenye vikao kwa wakati.

c)    Kuheshimu na kutekeleza maagizo halali kwenye vikao.

d)   Kushiriki kikamilifu katika shughuli zote halali na kuongeza kipato.

e)    Kubuni mbinu mbalimbali za kuboresha kikundi.

 

IBARA YA 13: UKOMO WA MWANACHAMA

Mwanakikundi atakoma kuwa mwanachama kwa:-

a)    Kifo.

b)   Kufukuzwa kwa utovu wa nidhamu.

c)    Kutolipa michango na hisa kwa kipindi cha miezi sita mfululizo bila ya sababu maalumu.

d)   Kutohudhuria vikao vitatu mfululizo bila ya taarifa.

e)    Kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi za kikundi mfano miradi ya kikundi.

f)     Kupata ugonjwa wa akili utakaothibitishwa na Daktari.

g)   Kujiuzuru mwenyewe kwa hiari yake.

 

 

 

IBARA 14: ADA YA MICHANGO YA WANACHAMA

a)   Kila mwanachama mpya anatakiwa kulipa ada ya kiingilio cha Tshs 50, 000/=

b)   Kila mwanachama atatakiwa kulipa michango mingine iliyoanishwa na kukubaliwa na wanachama wote.

c)   Kila mwanachama anatakiwa kulipa Hisa, thamani ya hisa moja itapangwa na kukubaliana na wanachama wote. Kiwango cha chini cha kununua hisa kuanzia hisa 1 na kiwango cha juu ni hisa 10. Mwanachama anaweza kutanguliza ununuzi wa hisa za ziada lakini asidaiwe hisa za nyuma.

d)   Kila mwanachama analazimika kuchangia Tshs 2500/= kwa wiki kama mchango wa mfuko wa jamii na elimu.

e)   Kila mwanachama atalazimika kuchangia kiasi cha pesa kitakachopangwa kwa ajili ya kumsaidia mwanachama mwenzetu atakayepata dharula pale inapobidi.

f)    Michango na ada itafanyika kupitia vikao vya vikundi.

 

IBARA 15: FAIDA ZITAKAZOPATIKANA

a)   Kujikwamua kiuchumi.

b)   Kumwezesha mwanachama kupata fedha kwa ajili ya matumizi yake.

c)   Kujenga uwezo wa kujiongezea kipato kwa wanakikundi.

SEHEMU YA 5: MUUNDO WA MAJUKUMU YA UONGOZI.

IBARA 16: UONGOZI WA KIKUNDI

Kikundi kitakuwa na uongozi ambao utasimamia shughuli zote zilizopo ndani ya kikundi kitakuwa na uongozi kwa mtiririko ufuatao:-

1.    Mwenyekiti.

2.    Katibu.

3.    Mweka hazina.

4.    Wajumbe watano

IBARA YA 16: 1: MAJUKUMU YA MWENYEKITI

Mwenyekiti atakuwa na majukumu yafuatayo:-

a)    Kusimamia/kuongoza mikutano ya kikundi.

b)   Kuweka sahihi kwenye fomu za mikopo na nyaraka za kikundi kwa ujumla.

c)    Kuitisha mikutano yote mikuu ya kikundi.

d)   Ni msemaji mkuu wa kikundi.

e)    Kukiwakilisha kikundi nje ya kikundi.

f)     Kujibu maswali na kutoa maelezo juu ya mambo mbali mbali katika mkutano mkuu.

IBARA 16: 2: MAJUKUMU YA KATIBU

Katibu atakuwa na majukumu yafuatayo:-

a)    Ni mtendaji/ mtekelezaji mkuu wa shughuli za kikundi.

b)   Mwenye kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za kikundi.

c)    Kumshauri mwenyekiti katika kazi za kila siku.

d)   Kuandaa kumbukumbu zote muhimu za kikundi pamoja na kumbukumbu za kifedha.

e)    Kufanya mawasiliano na wafadhili ( Serikali, Taasisi, NGOs, CBOs n.k)

f)     Kuitisha mikutano na kuandaa kama atakavyoagizwa na mwenyekiti.

g)   Kutekeleza maamuzi ya uongozi na mikutano ya wanakikundi.

h)   Ataweka sahihi kwenye fomu za mikopo na nyaraka nyingine za fedha na mali za kikundi kwa ujumla.

IBARA 16: 3: MAJUKUMU YA MWEKA HAZINA.

Mweka hazina atakuwa na majukumu yafuatayo:-

a)    Kutunza kumbukumbu zote ambazo zinahusu fedha za kikundi.

b)   Kupokea fedha na kuzitunza au kuziwasilisha zinapohusika kwa mujibu wa katiba na maelekezo wa wanakikundi.

c)    Kuandaa na kuwasilisha taarifa za fedha kwenye mkutano mkuu na kutoa ushauri wa matumizi ya fedha.

d)   Kufanya shughuli zote za fedha ambazo atapangiwa na kikundi ikiwa na pamoja na kuweka sahihi kwenye hundi na nyaraka nyingine za fedha.

IBARA YA 17: KAMATI TENDAJI

Kamati hii itafanya kazi mbalimbali za kikundi na itakuwa na wajumbe wafuatao:-

1.    Mwenyekiti.

2.    Katibu.

3.    Mweka hazina.

4.    Wajumbe watano miongoni mwa wanakikundi na kufanya kamati kuwa na wajumbe 8.

NB: Kamati hii inaweza kubadilika kutokana na ongezeko la wanachama.

 

 

 

 

IBARA 17: 1: MAJUKUMU YA KAMATI TENDAJI

a)    Kushughulikia na kuandaa mipango ya maendeleo ya kikundi.

b)   Kupokea na kujadili utekelezaji na maazimio ya mikutano yote ya kikundi.

c)    Kusimamia utekelezaji wa maamuzi ya mkutano mkuu na shughuli zote za kikundi.

d)   Kubuni na kupendekeza miradi na mbinu mbalimbali ya kuongeza pato la kikundi.

e)    Kushughulikia masuala yote ya mikopo na kuwasilisha taarifa hizo katika vikao vya kikundi.

f)     Kutataua migogoro na kero za kikundi.

 

IBARA 18: MUDA WA UKOMO WA UONGOZI

a)   Viongozi watakaochaguliwa watakaa madarakani kwa kipindi cha miaka mitatu  (3) tangia kuchaguliwa na wanaweza kugombea awamu nyingine kwa ridhaa ya wanachama.

b)   Kiongozi atakoma uongozi kwa kufukuzwa, kufariki, kuhama, kufungwa jela, zaidi ya mwaka mmoja (1), kurukwa na akili ama kujiuzuru mwenyewe.

c)   Kuondolewa na wanakikundi kwa kumpigia kura ya kutokuwa imani naye, maamuzi hayo lazima yafikiwe na wanakikundi wasiopungua ½ wanachama wote.

d)   Kutokuhudhuria vikao viwili bila taarifa na kukiuka onyo kwa kuendelea kutohudhuria vikaoni.

IBARA YA 19: MISINGI YA UENDESHAJI UCHAGUZI WA VIONGOZI

a)   Majina ya wagombea yatapendekezwa na wanachama au mwanachama kujipendekeza mwenyewe kwenye mkutano mkuu wa wanachama wote.

b)   Upigaji kura utakuwa  mtu mmoja kura moja na itakuwa ni siri na atakayepata kura za juu ndio atakuwa kiongozi / mshindi, endapo kura zitafungamana kura zitarudiwa mpaka apatikane mshindi.

c)   Utafanyika uchaguzi wa kujaza nafasi za uongozi zitakapoachwa wazi [pindi itakapojitokeza].

d)   Nafasi ilioachwa wazi Kaimu atakaimu kwa siku zisizozidi arobaini baada ya hapo lazima uchaguzi ufanyike

 

 

 

 

IBARA 20: MIIKO NA MAADILI YA VIONGOZI

a)    Kiongozi yeyote haruhusiwi kutumia madaraka yake kwa kutoa maamuzi ya kumnufaisha yeye binafsi, kutoa upendeleo kwa mtu yeyote kwa maslahi binafsi au kumkandamiza mtu yeyote.

b)   Ni kosa kwa kiongozi yeyote kutoa au kupokea rushwa ya aina yeyote kwa ajili ya kutoa huduma kwa mtu yeyote, adhabu yake ni kumfukuza uongozi.

c)    Asitoe siri za kikundi.

SEHEMU YA 6: MIKUTANO

IBARA YA 21: MKUTANO MKUU

Kutakuwa na mkutano mkuu ambao utahudhuriwa na wanachama wote ambao utafanyika mara mbili (2) kwa mwaka. Taarifa ya mkutano itatolewa ndani ya siku saba (7) kabla ya siku ya mkutano. Mkutano huu utajadili masuala ya kawaida ya maendeleo na kutatua changamoto za kikundi zilizoshindwa kufanyiwa kazi na kamati Tendaji. Pia mkutano mkuu ndio utakuwa na jukumu la kufanya maamuzi yote ya kikundi ikiwemo kupanga bajeti ya kikundi na kupokea taarifa ya fedha

 

IBARA 22: MKUTANO WA KAWAIDA

Kutakuwa na Mkutano wa kawaida wa wanachama wote utakaofanyika mara moja (1) kwa mwezi kwa lengo la kuwasilisha ada na michango mingine (jamii) pamoja na kujadili maendeleo ya kikundi.

 

IBARA YA 23: MKUTANO WA DHARULA

Kutakuwa na Mkutano wa dharula ambao utaitishwa pale itakapobidi au itakapotokea jambo lenye kuhitaji utatuzi wa haraka wa wanachama.

IBARA 24: UENDESHAJI WA MIKUTANO

Mkutano tajwa kwenye Ibara ya 21 – 23 itaendeshwa na Mwenyekiti na iwapo hatakuwepo wajumbe watachagua Mwenyekiti wa muda kutoka kwa wajumbe waliohudhuria. Maamuzi ya kikao yatakuwa halali iwapo ya theluthi mbili (2/2) ya wajumbe wote waliohudhuria kikao hicho. Iwapo mahudhurio hayatafika 2/3 kikao kitahairishwa na kuitishwa tena baada ya siku saba na wajumbe wakaohudhuria na kuridhia maamuzi yatakuwa halali hata kama mahudhurio yatakuwa hayajafika idadi inayotakiwa.

IBARA 25: VIKAO VYA KAMATI TENDAJI

Kamati tendaji itakutana kila mwezi mara moja (1) ili kujadili utekelezaji wa shughuli za kikundi na maagizo/ maamuzi ya mikutano ya wanachama wote kama inaweza kukutana wakati wowote inapotokea dharula.

SEHEMU YA 7: TARATIBU ZA FEDHA NA MALI ZA KIKUNDI

IBARA 26: MWAKA WA FEDHA

Mwaka wa fedha utaanza mwezi wa 4 (April) hadi mwezi wa 3 (March) ya kila mwaka.

Kikundi kitaamua kugawana faida au kitaendelea kutunza katika mfuko wa kikundi.

IBARA YA 27: VYANZO VYA MAPATO

Fedha / mapato ya kikundi yatatokana na: -

a)    Viingilio na michango ya wanachama.

b)   Mikopo toka Taasisi mbalimbali za fedha.

c)    Zawadi / ruzuku au misaada kutoka kwa wahisani.

d)   Mfuko wa jamii.

e)    Adhabu na faini kutoka kwa wanachama.

IBARA 28: HIFADHI YA FEDHA

a)    Kikundi kitafungua Akaunti Benki ambayo itaendeshwa na wanachama.

b)   Uendeshaji wa Akaunti utasimamiwa na Mwenyekiti, Mweka Hazina na wajumbe wawili.

c)    Kutakuwa na makundi mawili kundi A na kundi B. Kundi A atakuwa Mweka hazina na Mwenyekiti na kundi B atakuwa wajumbe wawili ambao ndio watia saini na kutoa fedha Benki. Watu wawili ndio wanaruhusiwa kutoa fedha, mmoja kutoka kundi A na mwingine kutoka kundi B wakiambatanisha muhtasari wa kikundi uliosaniwa na Mwenyekiti, Katibu sambamba na mahudhurio ya wanachama unaoonyesha makubaliano ya kuruhusiwa kufanya hivyo.

 

 

 

IBARA 29: MATUMIZI YA FEDHA

a)    Matumizi yote ya fedha za kikundi lazima yasizidi mapato na yataidhinishwa na kufanyika kwa utaratibu na kanuni zilizomo katika katiba hii.

HUDUMA ZITOLEWAZO NA KIKUNDI

MIKOPO

Mikopo itatolewa kwa wanachama wa kikundi hiki mara tu baada ya kumaliza mafunzo ya akiba na mikopo.

NB: MIKOPO YOTE HII ITAJADILIWA NA KUTOLEWA NA KAMATI TENDAJI NA KUWASILISHA TAARIFA KWA WANACHAMA KATIKA KILA KIKAO CHA KAWAIDA CHA WIKI.

MIKOPO ITATOLEWA KWA MASHARTI YAFUATAYO:-

(a)  Atajaza fomu ya maombi ya mkopo na atawasilisha maombi ya mkopo kwa kamati tendaji.

(b) Mkopo utajadiliwa na wanachama wote wa kikundi.

(c)  Mwombaji wa mkopo endapo atashindwa kulipa mkopo, hisa zake zitapunguzwa ili kulipia mkopo.

(d) Maombi ya mkopo yatajadiliwa na kupitishwa na wanakikundi wote.

(e)  Mikopo itakaoainishwa kwa madhumuni ya biashara, na kwa shughuli za kimaendeleo ya jamii kwa ujumla.

(f)   Hakutakuwa na mkopo mwingine utakaotolewa kwa mkopaji mwingine hadi pale deni la mkopo uliotangulia litakapokuwa limelipwa.

(g) Mkopo utatolewa kutokana na foleni ya wakopaji.

IWAPO MKOPO HAUTARUDISHWA KWA KIPINDI KILICHOWEKWA HATUA ZIFUATAZO ZITACHUKULIWA DHIDI YA MKOPAJI

a)   Muhusika aitwe na kuhojiwa mbele ya mkutano wa wanachama wote na atoe sababu zake.

b)   Ataweza kupewa muda wa mwezi mmoja (1) wa ziada ili aweze kumaliza deni kwa wakati.

c)   Muda wa ziada utakapokwisha na muhusika hakumaliza malipo basi hisa za mkopaji zitakatwa na kulipa deni

MCHANGO WA MFUKO WA JAMII

·         Kutakuwa na mfuko wa jamii ambao utachangwa na wanachama wa kikundi.

·         Mfuko wa jamii utatolewa kwa wiki mara moja.

·         Kima cha mchango kwa kila mwanachama kwa wiki  ni Tshs 2500/=

·         Endapo mwanachama hatalipa mchango wa Mfuko wa jamii hadi kufikia wiki ya mwisho wa mwezi mchango huo utakatwa katika Hisa zake.

MATUMIZI YA MFUKO WA JAMII

Mfuko wa jamii utatumika kuwapa wanachama watakaopatwa na matatizo yafuatayo:-

Kufariki kwa hawa wafuatao:-

a)    Baba au Mama Mzazi wa mwanachama atapewa pole ya Tshs 200, 000/=

b)   Mume au Mke wa mwanachama atapewa pole ya Tshs 200,000/=

c)    Mtoto wa kumzaa, mwanachama atachangiwa pole ya Tshs 200,000/=

d)   Kufariki kwa mwanachama wahusika watapewa pole ya Tshs 200,000/= pamoja na kurudishiwa michango yote alioichangwa kwa warithi wake

MFUKO WA JAMII HAUTAKOPESHWA ILA UTATOLEWA KWA KUAPA PALE WANACHAMA WATAKAPOPATA MAJANGA YASIYO TARAJIWA KAMA VILE:-

(a)  Mwanachama akipatwa na ajali au janga lolote wanakikundi watamchangia ili kumsaidia kwenye changamoto hiyo.

FAINI ZA MWANACHAMA

(a)  Kutohudhuria kikaoni bila ya taarifa faini itakuwa Tshs 5000/=

(b) Kuchelewa kufika kikaoni nusu saa tangu kikao kianze na haukutoa taarifa faini itakuwa Tshs 1000/=

(c)  Kuongea bila ya ruksa ya mwenyekiti faini itakuwa Tshs 200/=

 

IBARA 30: MGAWANYO WA MALI NA MAPATO

a)    Mali za kikundi ni pamoja na vitu vyote vinavyohamishika na visivyohamishika, vinavyomilikiwa na kikundi kama vile fedha na vitendea kazi. Mgao wa mapato utategemea mafanikio ya shughuli za kikundi na wanachama wake.

b)   Iwapo mwanachama amefariki, tathmini ya mali na mapato itafanyika na kupewa stahiki zake na kukabidhiwa mrithi wake atakayekuwa amemteua yeye mwenyewe kabla ya kufariki.

c)    Iwapo kikundi kitavunjika mali zote za kikundi watagaiwa wanachama baada ya kulipa madeni yote.

d)   Endapo mwanachama atajitoa mwenyewe kwa hiari yake ada yake atapewa baada ya mgao wa wanachama wengine.

SEHEMU YA 8: UTATUZI WA MIGOGORO NA UENDESHAJI WA KIKUNDI.

a)   Mwanachama hatatakiwa kutoa lugha ya kuudhi katika mkutano/ vikao dhidi ya wanachama wenzake.

b)   Mwanachama atakayeshindwa kuhudhuria vikao zaidi ya vitatu bila sababu za msingi atakuwa amejiondoa / amejifukuza mwenyewe.

c)   Mwanachama haruhusiwi kutoa siri ya kikundi, jambo lolote litakaloamuliwa ndani ya kikao itabaki kuwa siri.

UTARATIBU WA KUTATUA MIGOGORO KATIKA KIKUNDI NI:-

1.    Uongozi wa kikundi ndio wenye jukumu la kushughulikia migogoro yote itakayojitokeza, iwapo uongozi utashindwa kutatua utakuwepo mjadala wa wazi utakaohusisha wanachama halali wa kikundi kwa lengo la kutafuta suluhu na mwafaka wa jambo hilo, na endapo tatizo litaendelea hapana budi suala hilo kulifikisha katika ngazi nyingine za kiserikali ama za kisuluhisho ili kusaidia kutatua mgogoro huo.

SEHEMU YA 9: MAREKEBISHO / MABADILIKO YA KATIBA

Hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kubadili, kupunguza kipengele chochote ndani ya katiba hii.  Iwapo italazimika kufanya hivyo kulingana na wakati na mahitaji ya kikundi, mapendekezo ya kurekebisha au kubadili kipengele chochote cha katiba yatajadiliwa kwanza na uongozi wa kikundi na watatoa ushauri wa kurekebisha vipengele vya katiba katika Mkutano Mkuu ambao ndio una mamlaka ya juu kuidhinisha marekebisho ya katiba hii kwa kupiga kura iwapo maamuzi hayo yatafikiwa robo tatu (3/4) ya wanachama wote.

 

SEHEMU YA 10: KUVUNJIKA KWA KIKUNDI

Kikundi kinaweza kuvunjika kwa maoni ya ¾ ya wanachama wote baada ya kupiga kura katika Mkutano Mkuu wa mwaka au Mkutano wa dharula.

SEHEMU YA 11: HITIMISHO

Sisi wanachama wa kikundi cha DUBBING DEVELOPMENT GROUP tunakiri kwamba tumeshiriki kuandaa katiba hii hivyo tutailinda, kuitetea na kuifuata kama muongozo wetu katika shughuli zetu za kujiletea kipato kupitia kikundi chetu. Tunapenda kuthibitisha ushiriki wetu kwa kuambatanisha majina na sahihi zetu katika katiba hii.

 


  

© Copyright Tanzania Dubbing Artist Association-TDAA | Modified By Zotekali WEB Exparts
Back To Top